Genesis 40

Mnyweshaji Na Mwokaji

1Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2 aFarao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, 3 bakawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu. 4 cMkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia.

Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda,
5kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.

6Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. 7Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”

8 dWakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.”

Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”

9Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10 enao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. 11Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”

12 fYosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. 13 gKatika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake. 14 hLakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani. 15Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”

16 iYule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yosefu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yosefu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate. 17Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”

18 jYosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. 19 kKatika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”

20Mnamo siku ya tatu, ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake: 21 lNdipo akamrudisha mnyweshaji mkuu kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mikononi mwa Farao tena, 22lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, sawasawa na jinsi Yosefu alivyowaambia katika tafsiri yake.

23 mPamoja na hayo, mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yosefu, bali alimsahau.

Copyright information for SwhNEN